
TIMU ya soka ya Simba jana ilikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu bara baada ya kuifunga Stand United mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga.
Matokeo hayo yanaifanya Simba iongoze ligi kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu ikiwa na pointi 45 juu ya Yanga yenye pointi 43 na Azam yenye pointi 42. Hata hivyo Azam inaweza kurejea kileleni endapo itashinda mechi yake ya uwanja wa Mkwakwani Tanga dhidi ya Coastal Union itakayochezwa leo.
Yanga inayo nafasi kubwa ya kurejea kileleni kwani ina viporo. Mabingwa hao wa msimu uliopita wanatarajiwa kumenyana na Simba Februari 20. Mabao yote ya Simba yaliwekwa kimiani na Hamisi Kiiza katika dakika ya 34 na 47.
Kiiza sasa amefikisha mabao 16 na kuongoza orodha ya wafungaji kwenye ligi hiyo akifuatiwa na mshambuliaji wa Yanga Amisi Tambwe mwenye mabao 14. Bao la kufutia machozi la Stand United lilifungwa katika dakika ya 90 na David Osman.
Katika matokeo mengine ya ligi hiyo Kagera Sugar ilitoka sare ya bao 1-1 na JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Karume Dar es Salaam. Ruvu ilikuwa ya kwanza kupata bao lake katika dakika ya 22 kupitia kwa Nurdin Mohamed baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Saady Kipanga.
Dakika ya 71 Kagera Sugar ilifunga bao la kusawazisha kupitia kwa Ramadhan Kiparamoto. Kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Mbeya City ya huko iliifunga Toto Africans mabao 4-0.
chanzo:habarileo.
|