TIMU ya soka ya Mafunzo ya Zanzibar jana ilianza vibaya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa AS Vita ya Congo DR.
Tangu mwanzo wa kipindi cha kwanza cha mechi hiyo Mafunzo ilionekana kuelemewa karibu kila idara na kuruhusu wageni kutamba kana kwamba wanacheza nyumbani. Vita ilipata bao lake la kwanza katika dakika ya tano ya mchezo huo kupitia kwa Ikanga Mayimona baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Benard Morrison.
Mwamuzi wa mchezo huo aliamuru wageni wapige adhabu baada ya Emmanuel Ngudikana kuchezewa faulo na walinzi wa Mafunzo. Dakika ya 29 AS Vita walipata bao lingine mfungaji akiwa Ngudikana baada ya kuunganisha pasi ya Ngoda Muzinga na kuujaza mpira wavuni.
Dakika moja kabla ya kwenda mapumziko Muzinga aliifungia AS Vita bao la tatu. Dakika ya 79 wageni walipata penalti lakini mchezaji wake Benard Morrison alikosa baada ya kupiga mpira juu.
chanzo:habarileo.
|