Ndani ya dakika ya 44 ya mchezo huo, mchezaji wa Mafunzo Juma Othman Mmanga aliweza kumfanyia faulu mchezaji wa JKU Mbarouk Chande wakati alipokuwa kwenye harakati za kutaka kufuga bao ndani ya eneo la hatari, na ndipo mwamuzi wa pambano hilo Issa Haji alipoamua upigwe mkwaju wa penalt kuelekea kwenye lango la Mafunzo, lakini Mbarouk Chande alishindwa kuuzamisha wavuni mpira huo baada ya mlinda mlango wa Mafunzo Abdul-swamad Suleiman kuutoa mpira huo.
Katika kipindi cha pili timu zote ziliweza kufanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji wake lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuzaa matunda kwa timu zote kwani hadi mtanange huo ulipomalizika timu hizo zimetoka sare ya bila kufungana.
Timu hizo katika mzunguko wa mwanzo ziliweza kukutana na JKU waliweza kuwafunga Mafunzo mabao 2-1 katika ligi hiyo.
Mafunzo wakiwa ndio bingwa mtetezi wa ligi hiyo bado akionekana kususa msimu huu ambao wamepishana kwa alama kumi na tatu (13) na kinara wa ligi hiyo.
Kocha msaidizi Abdalla Bakar Eddo, amewataka mashabiki wake kuwa wasikate tama kwani taji hilo watalitetea bila ya wasiwasi wowote ule.
Kwa matokeo hayo timu ya JKU imebakia kileleni wakiwa na alama (32), huku bingwa mtetezi timu ya Mafunzo wao wakiwa nafasi ya saba na alama kumi na tisa (19).