
Timu ya Jang’ombe boys imeshindwa kutamba baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Kimbunga katika mchezo uliosukumwa jana jioni majira ya saa kumi ndani ya dimba la Amani mjini Zanzibar ambao ni muendelezo mwa ligi kuu ya Zanzibar kanda ya Unguja.
Katika mchezo huo uliojaa mashabiki kiwanjani timu hizo zilionesha kandanda safi kwa kufanya mashambulizi kila mara, na ndipo Waziri Ramadhan alipoweza kuipatia kimbunga bao la kuongoza katika dakika ya 28 ndani ya kipindi cha kwanza.
Bao la pili la Kimbunga liliweza kuwekwa kimyani na mchezi Khalfan Mgeni ndani ya dkika ya 58 ya kipindi cha pili mara baada ya pasi safi kutoka kwa Idrisa Simai, na kwa upande wa Jang’ombe boys bao la kufutia machozi lilifungwa na Abrahman Othman mnamo dakika ya 81 ya mchezo huo.

Katika mzunguko wa mwanzo timu hizo ziliweza kukutana na Jang’ombe boys walikubali kufungwa na Kimbunga mabao kama hayo 2-1, na wameweza kuendeleza tena uteja wao kwa Kimbunga baada ya jana kufungwa tena.
Kwa matokeo hayo Jang’ombe wapo nafasi ya tisa 9 na alama kumi na sita (16), huku Kimbunga wakipanda hadi nafasi ya nane (8) na alama zao ni kumi na saba (17).
|